Vous êtes sur la page 1sur 20

http://www.poetrytranslation.

org

POESIA SWAHILI

EUPHRASE KEZILAHABI
KITHAKA wa MBERIA
ALAMIN MAZRUI

INDICE
EUPHRASE KEZILAHABI
3 Upepo wa Wakati
4 Mafuriko
5 Mgomba
6 Chai ya Jioni
7 Fasihi
8 Kisima
KITHAKA wa MBERIA
9 Jumapili ya Damu
ALAMIN MAZRUI
12 Mlango
13 Mimi Ni Mimi
14 Nilivuka
15 Kifungoni
16 Kizuizini
17 Bega kwa bega
18 Sauti?
19 Mkata wa maneno
20 Niguse

EUPHRASE KEZILAHABI

Upepo wa Wakati
Juu ya mlima mdogo
Siku moja nilisimama.
Nikatazama chini ziwani, siku
Ya dhoruba. Halafu niliona mawimbi
Yakipanda na kushuka. Yakivimba,
Yakiviringika, yakigongana na kutoa povu
Kama fahari wehu katika bonde lisomajani.
Yalivyotengenezwa!
Yalivyofifia na kuanza tena!
Kamwe sikuona.
Lakini niliyaona yakishuka kwa nguvu
Na kupanda haraka, yakisukumwa
Na upepo wa Magharibi na Mashariki.
Hivyo ndivyo ulimwengu ulivyo.
Na hivyo maisha ya binadamu.
Wanapanda na kushuka
Wakisukumwa na upepo na wakati.
Tazama wanavyojinyakulia madaraka
Kama mzamaji, mguu wa rafikiye, ashikavyo!
Wanavyoshika pesa kama mtoto
Na picha ya bandia
Au asikari mwehu na bunduki yake
Na kutunyamazisha!
Watapanda na kushuka
Na wataanguka kweli!
Wakisukumwa na upepo wa wakati!

Mafuriko
Nitaandika wimbo juu ya mbawa za nzi
Utoe muziki arukapo wausikie walio wengi
Ushairi wa jalalani utaimbwa
Juu ya vidonda vya wakulima
Na usaha ulio jasho lao.
Nitaandika juu ya mbawa za wadudu
Wote warukao
Juu ya mistari ya pundamilia
Na masikio makubwa ya tembo.
Juu ya kuta vyooni, maofisini, madarasani,
Juu ya paa za nyumba, kuta za Ikulu,
Na juu ya khanga na tisheti.
Nitaandika wimbo huu:
Mafuriko ya mwaka huu
Yatishia nyumba kongwe bondeni.
Waliomo wameanza kuihama
Na miti ya umeme imeanguka.
Palipokuwa na mwanga, sasa giza.
Mafuriko ya mwaka huu!
Mti mkongwe umelalia upande
Wa nyumba zetu hafifu.
Upepo mkali uvumapo hatulali.
Kila kukicha twatazama mizizi yake
Na mkao wake, na kuta hafifu za nyumba.
Lazima ukatwe kuanzia matawi hadi shina
Mafuriko ya mwaka huu yaashiria...
Tutabaki kuwasimulia wajukuu:
Mwaka ule wa mafuriko
Miti mingi mikongwe ilianguka.
Mafuriko ya mwaka huu!
Wengi wataumbuka.

Mgomba
Mgomba umelala chini: hauna faida tena,
Baada ya kukatwa na wafanya kazi
Wa bustani kwa kusita.
Watoto, kwa wasiwasi wanasubiri wakati wao
Bustanini hakuna kitu
Isipokuwa upepo fulani wenye huzuni,
Unaotikisa majani na kutoa sauti ya kilio.
Hivyo ndivyo ufalme wa mitara ulivyo.
Mti wa mji umelala chini: hauna faida tena,
Baada ya kukatwa na wafanya kazi
Wa bustani kwa kusita.
Chumbani hakuna kitu
Isipokuwa upepo fulani wenye huzuni utingishao
Wenye hila waliokizunguka kitanda na kulia.
Machozi yenye matumaini yapiga
Mbiu ya hatari ya magomvi nyumbani.
Magomvi
Kati ya wanawake
Magomvi
Kati ya watoto kwa ajili ya vitu na uongozi.
Ole! Milki ya 'Lexanda imekwisha!

Vidonda vya ukoma visofunikwa


Ambavyo kwa mda mrefu vilifichama
Sasa viko nje kufyonzwa na inzi wa kila aina
Na vinanuka vibaya.
Lakini inzi kila mara hufyonza wakifikiri
Nani watamwambukiza.

Chai ya Jioni
Wakati tunywapo chai hapa upenuni
Na kuwatazama watoto wetu
Wakicheza bembea kwa furaha
Tujue kamba ya bembea yetu
Imeshalika na imeanza kuoza
Na bado kidogo tutaporomoka.
Kulikuwa na wakati ulinisukuma juu
Nikaenda zaidi ya nusu duara;
Kulikuwa na wakati nilikudaka
Ulipokaribia kuanguka,
Na kulikuwa na wakati tulibebana kwa zamu
Mmoja wima akisukuma mwingine amekaa.
Wakati huo, japo tulipaa mbele na nyuma
Tulicheka kwa matumaini yaliyotiwa chumvi
Na kisha tukaongozana jikoni kupika chajio;
Ilikuwa adhuhuri yetu.
Sasa tukisubiri ndoto tusizoweza kutekeleza tena
Tumalizie machicha ya chai yetu ya jioni
Bila kutematema na kwa tabasamu.
Baada ya hapo tujilambelambe utamuutamu
Uliobakia kwenye midomo yetu,
Tukikumbuka siku ilee ya kwanza
Tulipokutana jioni chini ya mwembe
Tukitafuta tawi zuri gumu
La kufunga bembea yetu
Naye mbwa Simba akikusubiri.
Lakini kabla hatujaondoka kimyakimya
Kukamilika nusu duara iliyobakia.
Tuhakikishe vikombe vyetu ni safi.

Fasihi
Maneno yangu kumeza tena sasa siwezi.
Lakini kuonyesha ukweli na kuutafuta
Nitaendelea: mimi ni kama boga.
Nimepandwa katikati, bustanini,
Na kama boga nitatambaa chini
Zote pande, kuikwea miti ya hekima
Na yote magugu koo kuyakaba.
Bila woga, bila nyuma kurudi nitashambulia
Ya binadamu matendo bado yakihema.
Halafu wakati
Ujao utafika
Matunda nitatoa
Makubwa madogo
Mazuri mabaya
Wakati utafika watakapokuja wajuzi
Kwa jembe la wino kunipalia.
Wala mboga za majani watanichuma.
Utafika, wa maboga kuwa mikata.
Machafu na safi yatachotwa
Na nitaingia mitungi ya kila mji-shamba.
Watoto mikononi mwao watanichezea.
Chini wataniangusha na kunipasua.
Lakini mbegu, mbegu zitabaki.
Mimi ninajua
Hatari sina
Wajibu msomaji
Mjini na shamba
Vizuri kunichambua.
Halafu utafika ule wakati
Watumia vikombe dhahabu na glasi
Pembeni kwa chuki kunitupa,
Na nitakuwa nyuma ya wakati
Lakini wakisahau wahenga
Kata na mboga walitumia
Msingi wa wao utamaduni
Watakuwa wameutupa.
Kumbukeni, kumbukeni, kumbukeni.

Kisima
Kisima cha maji ya uzima ki wazi
Na vyura katika bonde la taaluma watuita
Tujongee kwa mahadhi yao
Yaongozayo pandikizi la mtu
Kwa hatua ndefu litembealo
Na sindano ya shaba kitovuni
Upinde na mishale mkononi
Kisha likapiga goti kisimani
Tayari kumfuma akaribiaye
Maana shujaa hafi miongoni mwa wezi
Bali kama simba mawindoni.
Hatuwezi tena kuteka maji
Na kalamu zetu zimekauka wino.
Nani atamsukuma kwa kalamu
Aitwe shujaa wa uwongo!
Aliyeitia kitovuni kwa hofu
Ingawa tegemeo hakulipata
Alifungua mlango uelekeao
Katikati ya ujuzi na urazini mpya
Mwanzo wa kizazi tukionacho.

KITHAKA wa MBERIA

Jumapili ya Damu
I
Midundo ya Reggae
Inarindima hewani
Na kuchanganyika
Na macheo

Katika jiji
Vioo, madirisha
Na milango
Inasalimu amri
Kutoka kumbo kali
Za wenye njaa
Na matarajio
Ya miongo miwili.

Ndani ya maduka
Mawimbi ya watu
Yanapaa, kushuka
Na kupanda kwingineko
Huku rafu na kuta
Zikibadilika sura
Kama tanzu za miti
Kiangazi kinapojiri.

Vifaa vya kila ukoo


Nguo za kila rangi
Zinaketi vichwani
Kuninginia mikononi
Kulala migongoni
Au kubanwa kwapani
Zikibadili makazi
Na umiliki.

II

Risasi
Zinaanza kupiga miluzi
Na kwa ghadhabu
Kushtua kuta
Milingoti ya stima
Magari ya rangirangi
Na nyama na mifupa

Watu wanaterereka
Damu inatiririka
Uhai unaporomoka

III

Ghafla
Midundo ya Reggae
Inakauka
Na nyimbo za jana
Kurudi angani
Kama uvundo ambao
Umevamia pua tena
Baada ya kuangushwa
Na kumbo la upepo

Kutoka mwangu jikoni


Barabara ni dhahiriMagari ya rangirangi
Vifaru vya madoadoa
Vinatiririka kama mto,
Bunduki zinalenga kushoto
Kulia, nyuma na mbele
Nayo mizinga hatari
Inatega mbingu;
Huu mtiririko
Ni safari ya marejeo
Anarejea mungu-wa-kinamo
Kwenye ulingo.

IV

Katika fahamu
Mawazo mbalimbali
Yanapita kwa zamu
Kama vipepeo na nondo
Wakipita kwa makundi
Mbele ya macho;
Kwa tabasamu
Nakumbuka Obasanjo
Na uamuzi wake angavu
Bali pia
Kwa huzuni
Nakumbuka Bokassa na Amin,
Na Mobutu na Doe,
Na damu na mafuvu
Matita ya mafuvu!
Magurudumu ya mawazo
Yanafikia njia panda
Na kwa muda, kukwama
Kabla ya kuanza safari tena
Kwenye njia wazi
Ya serikali ya kiraia
Hata inapoongozwa
Na genge la mazimwi

ALAMIN MAZRUI
Alamin Mazrui

Mlango
Ama utapita
katika mlango huu
au hutapita.
Ukipita
kuna hatari
ya jinalo kulisahau.
Hayo ni matata
Mambo hukutizama mara mbili mbili
Nawe sharuti utazame kando
uwache yatendeke.
Usitafute vita.
Usipopita
Huenda ukakuta
maisha mema ya kufuata
ukahifadhi mawazo yako
ukaendelea na kazi yako
ukafa kishujaa nchini mwako
lakini mengi huenda yakakupita
mengi yakakupofua, upofu ukakupata
kwa gharama gani? Sijui.
Mlango wenyewe
haumuahidi mtu kitu
Ni mlango tu!

Mimi Ni Mimi
Waniita mkomunisti
Waniita mkapitalisti
Waniita mnashinalisti
Na mimi ni binadamu tu,
Kwani hilo halitoshi?

Nchi zinajiwakia
Mamama wakiomboleza, wakilia
Tumbi ya watoto wakiumia
na maneno yote tunayotumia
kuuana na kuangamia

Ewe mto
Tumesimama pambizoni mwako
machozi yakitudondoka
yakichanganyika moyoni mwako.

Nilivuka
Nimevuka mabara kuja Afrika
Lakini siku katu haikufika
ya milima kuwa vilima
ya mito kuwa vijito
vya kuweza kudakiika.
Sijakufikia mpenzi
kama kwamba u nyota ya mbali
kama kwamba umemea baina yetu
ukuta wa usingizi.
Nikikushika, mikono huwa haishiki
ila maiti ilokufa bila haki
kama kukumbatia damu yangu jiweni
katika nyumba iloghariki kwa tufani
ambayo usiku wake umesimama makini
na asubuhi yake imekwama mbali
ikisubiri njiani.

Miaka imenyumbuka baina yetu: damu na moto,


Daraja nikazikwea zilogeuka ukuta
Na wewe, ukazama chini baharini
nisiweze kukugusa.
Mashaza yakanichuna, yakikata mishipa
ya mikono yangu,
Nami nikaita:
Ewe Afrika
mpenzi wa roho yangu,
mwenzi wa mabuu na giza,
Nimezunguka miaka mingi kukutafuta
na safari yangu bado haijakatika
ewe maiti ulojifinika kwa yako maisha.

Nimevuka mabara kuja Afrika


lakini siku katu haikufika
ya daraja kuweza kuvukika.
Ewe ulalaye nami kitandani
U kama nyota ya mbali mbinguni
ulo milango ilofungwa kwa ndani
Nami nimesimama nje
nasubiri baridini.

Kifungoni
Kwa kuangulia juu mbinguni
na kulia sana kwa matumaini
samawati imeingia
mwangu machoni.
Kwa kuota mahindi mashambani
na kulia sana kwa mahuzuni
manjano imeingia
mwangu machoni.

Waache majemadari waende vitani


Wapenzi waende bustanini
Na waalimu mwao darasani,
Ama mimi, tasubihi nipeni
Na kiti cha kale, za zamani
Niwe vivi nilivyo duniani:
bawabu mlangoni
katika kingo ya maumivu ya ndani
maadamu vitabu, sheria na zote dini
zitanihakikishia mauti
nikiwa na njaa au kifungoni.

Kizuizini
Nikiwa na njaa na matambara mwilini
nimehudumika kama hayawani
Kupigwa na kutukanwa
kimya kama kupita kwa shetani.
Nafasi ya kupumzika hakuna
ya kulala hakuna
ya kuwaza hakuna.
Basi kwani hili kufanyika.
Ni kosa gani lilotendeka
Liloniletea adhabu hii isomalizika?
Ewe mwewe urukae juu mbinguni
wajua lililomo mwangu moyoni.
Niambie: pale mipunga inapopepea
ikitema miale ya jua
Mamaangu bado angali amesimama akinisubiri?
Je nadhari yake hujitokeza usoni
ikielekea huku kizuizini?
Mpenzi mama, nitarudi nyumbani
Nitarudi kama hata ni kifoni
Hata kama maiti yangu imekatikakatika
vipande elfu, elfu kumi
Nitarudi nyumbani
Nikipenya kwenye ukuta huu
nikipitia mwingine kama shetani,
Nitarudi mpenzi mama ....
hata kama ni kifoni.

Bega kwa bega


Baridi kutoka mlima mwa Kenya inaingia
Na upepo unavuma, misitu ya Nyandarua ukipasua
Lakini mimi ni mwanamke wa Kirinyaga
baridi sitaisikia
chochote sitakisikia
isipokuwa sauti ya ardhi yetu
nchi yetu
polepole ikinililia.
Nyumbani...
kuponda unga kunatusubiri
kuchuna mboga kunatusubiri
kuchanja kuni kunatusubiri
na watoto
watoto si haba
nao pia wanatusubiri.
Lakini kumfuata mume wangu naendelea
nchi yangu kuipigania
utu wangu kujirudishia.
Lala mwanangu lala
lala unono ukinisubiri.
Mwezi utakapoinama
nitarudi, nikulinde nikuamiri
Juu ya milima
mwezi umejaa, umechotama
kwa huruma ukitutazama.
Njia ni ndefu mno
Muda ni mfupi mno
lakini kumfuata mume wangu naendelea
bega kwa bega nasogea
utu kuukomboa.

Sauti?
Shingo zetu zimechongoka
asubuhi kuilekea
lakini usiku wasogea
ukichimba misingi ya nyumba,
na ukuta wa dakika nyumba
kuizunguka.

Kifo kimeadhimishwa
na ule wakati uliotandazika
mpaka
kila cha zamani kimesahaulika
isipokuwa majani makavu yalokauka
Mitini, mara kwa mara, yakitingisika

Ati n'nani aliyesikia sauti?


Kama kwamba kuna mtu huko mbinguni
wa kutulipia damu yetu iliyomwagwa
na kumwagika

Mkata wa maneno
Zacheka nami zangu chekeo
zacheka zafurahika
Sina mawazo kichwani leo
Bado hayajarauka ...

Nadhani ni asubuhi
imeanza kuchipuka
Nayo ndiyo sababu
ya moyo kuliwazika
na huu mdundo mtamu
mwema ulotandazika

Najichekea ... kwani najua vyema


kwamba sijazoea hali hii tabasama
ijitembezayo kwa shairi na kwa ngoma
ikichezacheza nami ... ikininyegeza kama mke na mume
kama wapenzi daima

Najua sijaizoea hali hii ya furaha na shauku


ijigambayo kwa mchana na usiku
kufuata mtindo wa manju kila siku
... kufuata anasa za dunia

Ndipo nikawa mkata...


mkata wa maneno ya furaha na amani
ya mahaba au dini
maneno ya kufifisha kisasi cha mja
juu ya maisha duniani
maneno ya kushinda vita vya nyoyoni
hivyo vita vya ndani kwa ndani.

Neno langu ni maumivu tu, ni mashaka


Ndipo kapendelea mwenendo wa kale ...
fikira kutoziandika.

Niguse
Nitakapo kizuizini
Nitamwomba yoyote mwendani
aniguse
taratibu
polepole
lakini
kwa yakini!

Niguse tena
Unijuze tena
Unifunze tena
maisha yalivyo
maisha yaonjavyo
ladha yake ilivyo

Nipo hapa nimekukabili


Niguse tena tafadhali!
Niguse!
Niguse!

UNF O

Lanciato il 9/1/2016

Vous aimerez peut-être aussi